BRYSON MSHANA, NANYUMBU
mtwarapressclub@gmail.com
Mnada wa kwanza wa ununuzi wa Korosho Msimu 2023/2024, umefanyika Octoba 20,2023 katika Kijiji cha Mburusa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara, huku kampuni zaidi ya 30 zikijitokeza kuonesha nia ya kununua Korosho katika mnada huo.
Jumala ya Tani za korosho 10,000 zimeuzwa kwa bei ya kati ya shilingi 2,032 ikiwa ni bei ya juu na 1,900 ambayo ni bei ya chini, huku kiasi chote cha Korosho kilichopelekwa mnadani kikifanikiwa kununuliwa katika siku hiyo ya kwanza ya mnada.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU Biadia Matipa, ameeleza kuwa Matarajio ya msimu huu ni kuuza Korosho kwa bei nzuri kulingana na soko la Dunia lilivyo kwa sasa, pamoja na kuwa bei zilizoanzia leo ziko chini ikilinganishwa na zile za msimu uliopita.
Ameeleza kuwa wanaendelea kufanya mawasiliano na wanunuzi ili wajitokeze zaidi, lakini pia wana kufuatilia mwenendo wa bei ya zao hilo ulivyo katika maeneo mengine Duniani.
Biadia amesema kuwa matarajio ya msimu huu ni uzalishaji wa kutosha unaokadiriwa kufikia tani elfu 80, kutokana na wingi wa pembejeo ambazo zimetolewa na Serikali.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Dkt.Izack Mwakajumlo amewataka wakulima kutumia vizuri fedha watakazozipata katika uuzaji wa Korosho, ili ziweze kuwasaidia katika mambo mbalimbali ya maendeleo.

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Dkt.Izack Mwakajumlo akizungumza na Wakulima wakati wa ufunguzi wa mnada wa kwanza wa ununuzi wa Korosho Msimu 2023/2024 katika Kijiji cha Mburusa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Octoba 20,2023 (PICHA NA MAHMOUD ISSA)
Amesema kuwa Serikali imaendelea kuwajali wakulima na kufuatilia masoko zaidi ili kiwavutia wanunuzi wengine watakaozidisha udhindani na kupandisha bei.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Bw. Francis Alfred amewapongeza wakulima waliojitokeza na mnadani na kuamua kuuza Korosho, akieleza kuwa bei iliyowasilishwa inaashiria uhalisia wa bei zilivyo katika soko la Dunia.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Bw. Francis Alfred, akizungumza na Wakulima wakati wa ufunguzi wa mnada wa kwanza wa ununuzi wa Korosho Msimu 2023/2024 katika Kijiji cha Mburusa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Octoba 20,2023 (PICHA NA MAHMOUD ISSA)
Kuhusu bei hiyo kuendelea kushuka ikilinganishwa na Msimu uliopita, Francis amesema CBT kama msimamizi mkuu wa Tasnia wanaendelea kushughulikia mwenendo huo ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa ukaribu hali halisi ya soko lilivyo kimataifa.
“Niwashukuru wakulima kwa kufikia uamuzi wa kuuza Korosho zao, kwa sababu kiuhalisia bei waliyouza ndivyo hali ya soko ilivyo katika soko la kimataifa, hali ya soko katika dunia ndiyo inatafsiri hali ya soko katika nchi yetu” amesisitiza Alfred.

Baadhi ya wakulima wa zao la Korosho waliojitokeza katika mnada wa kwanza wa ununuzi wa Korosho Msimu 2023/2024 katika Kijiji cha Mburusa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Octoba 20, 2023 (PICHA NA MAHMOUD ISSA)
Akizungumza kwa niaba ya wakulima waliohudhuria mnada huo ulioshirikisha Jumla ya Makampuni 33 yalijitokea katika mnada wa leo, Bi Mwanaisha Juma ambaye ni mkulima wa korosho kutoka kijiji cha Mburusa Wilaya ya Nanyumbu, ameeleza kuwa wamelazimika kuuza Korosho zao kwa sababu ya halihalisi ya soko waliyoisikia kutoka kwa wataalam waliokuwa kwenye mnada.
“Hii sio bei tuliyoitarajia lakini kwa maelezo yale yaliyotolewa ya mwenendo wa bei huko Duniani hata tukisema tusiuze tutazipeleka wapi wakati wanunuzi ni walewale? Alihoji Bi Mwanaisha
“Tunachoeza kuomba hapa ni Serikali kuona namna ya kutafuta namna ya kuokoa zao hili katika miaka inayokuja, maana kama bei zitaendelea kuwa hivi zitazidi kuwaumiza wakulima ambao wanatumia muda na gharama shambani jambo ambalo linakatisha tama” ameongeza

Baadhi ya wakulima wa zao la Korosho wakishuhudia ufunguzi wa sanduku lenye barua za kampuni zilizooomba kununua Korosho katika katika mnada wa ununuzi wa Korosho uliofanyika katika Kijiji cha Mburusa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Octoba 20, 2023 (PICHA NA MAHMOUD ISSA)
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






