BRYSON MSHANA, DAR ES SALAAM
mtwarapressclub@gmail.com
Bodi ya Korosho Tanzania imeeleza kuwa imepokea na itayafanyia maagizo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango aliyoyatoa wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa zao la korosho Octoba 11, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya CBT Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile, ameeleza kuwa maagizo yaliyotolewa na Dkt. Mpango ya kutaka Korosho zinazozalishwa Tanzania zibanguliwe hapa nchini yanaenda sambamba na mipango ya CBT iliyoiweka hivyo kinachofanyika hivi sasa ni kuharakisha taratibu mbalimbali ili utekelezaji uanze.
Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile, alikuwa akizungumza katika siku ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho Jijini Dar es salaam, na kusisitiza kuwa Bodi anayoiongoza itahakikisha kuwa mipango ya Serikali ya kuendeleza sekta ya Korosho inafanikiwa kwa wakati.
“Leo ni siku ya pili ya Mkutano huu, kesho tarehe 13 hatutakuwa ukumbini tutaenda kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuwaonesha wageni wetu fursa zitokanazo na zao la Korosho hapa nchini ikiwepo uwekezaji, hivyo niseme kuwa maagizi aliyoyatoa Makamu wa Rais yanafanyiwa kazi kwa vitendo” Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa CBT Bw. Francis Alfred amewashukuru wadau wote walioshiriki katika kuhakikisha kuwa mkutano huo wa kihistoria unafanyika kwa mafanikio makubwa na kuipa heshima Tasnia ya Korosho.
Amesema Mkutano huo umeandika historia kubwa kwa Tasnia ya Korosho na Taifa kwa ujumla, na kilichobaki hivi sasa ni kutekeleza yale yote yaliyopo kwenye mipango hususan eneo la kuongeza uzalishaji na kuwezesha ubanguaji ili kuongeza thamani ya zao kwa ajili ya kumnufaisha mkulima na kukuza uchumi wa Nchi.
“Tumefanya Mkutano huu sio kwa uwezo wetu wenyewe, bali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliopo kwenye sekta ya Korosho, niendelee kuwakaribisha tushirikiane katika shughuli na matukio mbalimbali ya kukuza na kuendelea tasnia ya Korosho katika nchi yetu” amesema Alfred.
Mkutano wa Kimataifa wa zao la korosho unafanyika kwa mara ya kwanza nchini, ukijumuisha zaidi ya wadau 500 kutoka nchi 33 zinazozalisha na kula korosho ukielezwa kuwa ni fursa ya kipekee kwa nchi ya Tanzania kuweza kujitangaza kimataifa kuhusu uwezo wake mkubwa uzalishaji wa korosho bora Duniani.
Mapema wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Octoba 11, 2023 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo ba Mifugo, Mariam Ditopile Mzuzuri, alisema ni ishara ya Tanzania kuendelea kuvutia Mataifa mengine duniani kutokana na kuwa na sera nzuri za uwekezaji hususan katika kilimo cha korosho.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






