BRYSON MSHANA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Muhogo ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula nchini Tanzania ikikadiriwa kuwa zaidi ya tani milioni nane (8) za muhogo mbichi zinazalishwa nchini kwa mwaka.

Kanda ya ziwa inaongoza kwa uzalishaji wa Muhogo kwa (37%), ikifuatiwa na Kanda ya Kusini (28%) na Kanda ya Mashariki (12%), huku 75% ya muhogo unaozalishwa ukiwa unatumika kwa ajiji ya chakula.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI-Naliendelea iliyo Mkoani Mtwara, imekuwa ikifanya utafiti wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara, kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wakulima wanalima kisasa na kutumia mbegu bora ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi.

TARI Kituo cha Naliendele Mtwara, imewekeza katika kutafiti pamoja na kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali kama Korosho, Ufuta, Karanga, Mihogo, Matunda pamoja na Mbogamboga, hivyo kuwa msaada kwa wakulima wanaolima mazao hayo nchini.

Mtafiti muandamizi wa zao la Muhogo kutoka TARI Kituo cha Naliendele Bi Bernadetha Pondamali Kimata, anauelezea zao hilo kuwa ni chakula kikuu cha wananchi wa mikoa ya kusini mwa Tanzania na wananchi wamekuwa wakihamasika kufanya kilimo hicho kwa wingi.

Bi Kimata anasema kuwa hamasa ya wananchi imetokana na uwepo wa mbegu za kisasa zilizotafitiwa na kuzalishwa na TARI, ambazo zimeongeza uzalishaji hivyo kuwavutia wananchi wengi kuingia katika kilimo cha muhogo kwa ajili ya chakula na biashara.

“Matumizi ya mbegu bora zaidi ya 13 zilizozalishwa kitaalam yamechangia kuongeza uzalishaji wa hadi tani 8 kwa heka 1 hivyo mkulima anakuwa na uhakika wa mavuno ya uhakika ambayo yanamsaidia kupata chakula lakini pia kuuza kwa ajili ya kuongeza kipato” anaongeza Bi Bernadeta Kimata.

Akielezea faida za mbegu bora zilizotafitiwa kitaalam, anasema kuwa zinavumilia magonjwa na wanaendelea program ya kuwafundisha wakulama katika maeneo mbalimbali ili waweze kufanya uzalishaji wa mbegu kwa ajili ya kuongeza wigo wa kuwafikia wahitaji wengi zaidi.

Vilevile Bi Bernadeta Kimata anaamini kuwa ongezeko la uzalishaji wa zao la Muhogo katika mikoa ya kusini linapaswa kuendana na kazi ya uwekezaji hususan viwanda vidogo na vikubwa, ambavyo vitasaidia katika kuliongezea thamani zao hilo.

“Tunaendelea kutafiti na kuzalisha mbegu bora zaidi kwa ajili ya kuwafikia wakulima wengi zaidi, hali hii inaendana na ongezeko la uzalishaji ambalo linahitaji kuwekeza zaidi ili kuliongezea thamani zao kwa kuongeza mnyororo wa tahamni kupitia uwepo wa viwanda katika maeneo ya wakulima” amesisitiza Bi Kimata.

Kwa upande wake Mtafiti wa Mazao ya Mizizi na Viazi kutoka Festo Massira, anasema kuwa bado kuna muamko mdogo wa wadau wengine kujitokeza kujifunza namna ya kuzalisha mbegu mbalimbali akieleza kuwa hiyo ni fursa nyingine ambayo wananchi wanaweza kuitumia katika kujiongezea kipato.

TARI Kituo cha Naliendele tunao wataalam wa kutosha kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wadau wengine kuweza kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali ukiwepo muhogo, tukishakujengea uwezo unaenda kuzalisha kitaalam na kuuzia wengine ili kukuza zao lakini pia kujipatia kipata”

“ Wananchi, Taasisi na Jumuia mbalimbali kutoka mikoa hii ya kusini zinaweza kufika katika vituo vyetu kwa ajili ya kupata maelekezo zaidi juu ya namna wanavyoweza kushiriki katika kuzalisha mbegu kitaalam” Festo Massira

Mikakati hii ya TARI katika kuendeleza zao la Muhogo mikoa ya Kusini na Tanzania kwa ujumla, inaenda sambamba na mazingira mazuri ambayo yamewekwa na Serikali kuhakikisha kuwa sekta kilimo nchini inazidi kukua.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas anasema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza kwenye kilimo bora na chenye tija ambacho sio tu kwamba kitamfaa mkulima kwa chakula lakini pia aweze kupata soko la uhakika na kujiingizia kipato.

Akizungumza Agusti 06, 2023 kwenye maonesho ya Mbegu za Asili Kanda ya Kusini 2023, yaliyoandaliwa na Shirika la SWISSAID Tanzania kwenye viwanja vya maeonesho ya Wakulima na wafugaji Nanenane eneo la Ngongo Manispaa ya Mkoani Lindi, Kanali Abbas alisema Serikali ya awamu ya sita imeonesha nia ya dhati ya kutaka kumkomboa mkulima kupitia kilimo bora.

“Mazingira mazuri ambayo Serikali imeyaweka katika sekta ya kilimo, yameongeza hamasa kwa wananchi wa mikoa ya kusini kuzidi kuingia kwenye kilimo cha Korosho, Ufuta, Mbaazi, Choroko, Muhogo, mbogamboga pamoja na matunda”

“Na kuonesha hilo ndio maana taasisi zetu za utafiti wa kilimo kama TARI zimeendelea kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya kutafiti zaidi na kuzalisha kwa wingi mbegu bora ambazo zitaenda kuwasaidia wananchi kwa kuongeza mazao yao na kupata soko la uhakika” amesema Kanali Abbas.

 

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…