BRYSON MSHANA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmedi Abbas, amewakaribisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza mkoani humo kutokana na kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji.

Kanali Abbas amesema hayo August 5, 2023 wakati aliposhiriki katika tukio la kitalii lililohusisha uzinduzi wa msimu wa utalii wa Nyangumi katika eneo la Bahari lililopo Luvula – Msimbati Mkoani Mtwara.

Amesema kuwa Mtwara ni moja ya maeneo yenye mazingira rafiki kwa uwekezaji hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa usalama, hivyo wawekezaji hawaa budi kujitokeza kwa wingi ili kuwekeza hususan kwenye sekta ya utalii.

“Tumeendelea kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji katika mkoa wetu, na ndio maana hata leo tupo hapa kushuhudia msimu huu wa nyangumi, huu ni utalii na nichukue nafasi hii kuwakaribisha wananchi kutembelea eneo hili”

“Vilevile hii ni fursa kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya utalii hasa wa baharini,sisi mkoa tupo vizuri tumeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo  ni rafiki kwa kila mtu”

“Wawekezaji waje kujenga Mahoteli, waje kufanya uwekezaji safari za boti za kubeba wageni kuwapeleka maeneo mbali mbali ya vivutio vya utalii vilivyopo katika ukanda huu wa bahari eneo la Mtwara” amesisitiza Kanali Abasi.

Kwa upande wake afisa Muhifadhi Mfawidhi wa Hifadhi ya Bahari ya huba ya Mnazibay na maingilio ya Mto Ruvuma Redfrey Ngowo, amesema kuwa eneo la hifadhi lina ukubwa wa kilomita za mraba 650 ambapo kati ya hizo kilomita 430 ni eneo la maji wanapopatikana Nyangumi.

Amesema Nyangumi hao wamekuwa kivutio kikubwa cha watalii kutembelea eneo hilo, akieleza kuwa zaidi ya watalii 560 kwa mwaka 2022,  watalii 630 kwa mwaka 2023 wametembelea eneo hilo.

Ngowo amesema kuwa Nyangumi ana uwezo wa kutambua mazingira rafiki kwa kuishi hivyo kutokana na kuongezeka kwa hali baridi ya Bahari ya kusini Mwa afrika, kila mwaka ifikapo mwezi july hadi November wamekuwa wakipatiana katika eneo la Msimbati Mkoani Mtwara

Naye Bi Esha Chilonda ambaye ni afisa mtendaji wa kata ya Msimbati amesema kuwa msimabati ni eneo lililo barikiwa na uwepo wa vivutio mbalimbali ikiwemo Milima ya Mchanga, fukwe za kuvutia na visima vya Gesi Asilia.

Vilevile amewataja viumbe wa Bahari kuwa sehemu ya vivutio vya eneo hilo, hivyo kuwataka wananchi kuwa tayari kupokea wageni wakati wote.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…