BRYSON MSHANA, LINDI

www.mtwarapressblog.co.tz

Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC), kinaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa uwekezaji unazidi kuimarika ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira rafiki, kinaibua na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana Tanzania.

Katika kuhakikisha kuwa jitihada hizo zinafanikiwa, TIC imeeleza kuwa itaanza kukutana wakuu wa Mikoa mbalimbali nchini kwa kuwatembelea na kujadiliana juu ya namna nzuri ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo yao.

Akizungumza Agusti 06, 2023 kwenye Banda la TIC wakati wa maonesho ya wakulima na wafugaji Nanenane Kanda ya Kusini yanayofanyika katika viwanja vya Ngongo Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi, Meneja Muwezeshaji Uwekezaji wa TIC Bi. Grace Lemunge ameeleza kuwa huo ni sehemu ya mkakati wa Kituo kukuza uwekezaji nchini.

“Tunatarajia kufika kila mkoa kukutana na viongozi wa mikoa hiyo ili kujadiliana na kuweka mipango ya pamoja itakayowezesha kukuza uwekezaji kwa manufaa ya Taifa letu la Tanzania” ameeleza Bi Lemunge

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanal Ahmed Abbas ambaye alitembelea Banda la TIC Agusti 06, 2023, ameeleza kuwa Mikoa ya Kusini mwa Tanzania inazo fursa nyingi za uwekezaji ambazo Serikali kupitia kituo cha uwekezaji inaweza kuona namna ya kuzielezea zaidi katika majukwaa mbalimbali.

Kanali Abbas ameipongeza TIC kwa namna inavyofanya kazi huku akiitaka kuendelea na juhudi hizo ili kuunga mkono kwa vitendo azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akiitangaza Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani kuwa sehemu salama ya kwa wakezaji.

“Mhe.Rais DKT Samia Suluhu Hassana amefanya juhudi kubwa sana za kuitangaza nchi yetu maeneo yote Duniani, hii imewafanya wawekezaji wakubwa kuvutiwa kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa Tanzania, hivyo TIC inapaswa kuhakikisha kuwa haimuangushi Mhe Raisi wetu” amesisitiza Kanali Abbas.

Kituo cha uwekezaji Tanzania kinashiriki Maonesho ya Nananenane Kanda ya kusini, ambapo wananchi, viongozi na wadau mbalimbali wamekuwa wakitumia fursa hiyo kupata elimu juu ya kazi za kituo hicho pamoja na namna kinavyotekeleza majukumu yake.

Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane Kanda ya kusini, yalifunguliwa rasmi Tarehe 1 Agusti 2023, na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sigini, yakiwa na kauli mbiu inayosema, Vijana na Wanawake, ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula”.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…