MWANDISHI WETU, DODOMA

mtwarapressclub@gmail.com

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekua sehemu ya Taasisi zilizozindua mkataba wa Huduma kwa Mteja ili kuwezesha wananchi kuwa na uelewa juu ya huduma zinazotolewa na Wakala lakini pia namna ya kupata haki na huduma mbalimbali.

Akizindua mikataba ya Huduma kwa Mteja ya Taasisi za Umma katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameeleza kuwa licha ya kuwa na mikataba ya huduma kwa mteja watumishi wa umma wanatakiwa kuhakikisha wanatenda haki kwa wakati kulingana na mikataba inavyoelekeza.

Aidha amewasisitiza waajiri kuhakikisha wanatenda haki kwa watumishi ili kuwezesha watumishi kuwa na utulivu na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa huduma kwa wananchi lazima zitolewe kwa wakati kwa kuangalia kanuni na taratibu lakini pia wakati mwingine kutumia hekima na busara ili kuhakikisha lengo la utoaji wa huduma linakamilika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TARURA Bi. Azimina Mbilinyi ameeleza kuwa mkataba wa huduma kwa mteja utasaidia katika kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kasi lakini pia utawezesha wananchi kutoa mrejesho na maoni mbalimbali kwa wakati.

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) utaendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia mkataba wa huduma kwa mteja ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa wakati.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…