Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua jengo la dharura kwenye hospitali ya wilaya ya Ruangwa, Machi 31, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa  Afisa Muuguzi Shifra Buroko kuhusu mashine ya usaidizi ya kupumulia baada ya kuzindua Jengo la  Wagonjwa wa Dharura la Hospitali ya wilaya ya Ruangwa, Machi , 31, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa  Dkt. Mohamed Amri kuhusu mashine ya kuamshia mapigo ya moyo ‘defibrillaor’ baada ya kuzindua  Jengo la  Wagonjwa wa Dharura la Hospitali ya wilaya ya Ruangwa , Machi , 31, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
OFISI YA WAZIRIK MKUU, RUANGWA
mtwarapressclub@gmail.com

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua jengo la wagonjwa wa dharura kwenye hospitali ya wilaya ya Ruangwa ambalo limegharimu sh. milioni 390.

Akizungumza na wakazi wa Ruangwa waliofika kushuhudia uzinduzi huo Machi 31, 2023, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ujenzi huo na hasa kwa vile amekuta kuna vifaa vya kisasa.

“Yote haya ni matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na yamesaidia kuifanya wilaya yetu iwe miongoni mwa wilaya zinazoenda kwa kasi,” amesema.
Waziri Mkuu amesema hospitali hiyo imejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 100 ambalo kazi ya kujenga uzio ni kubwa kwa hiyo akawataka wakazi hao wawe walinzi wa miundombinu na vifaa tiba vilivyonunuliwa ili waendelee kupata huduma bora na za uhakika.

“Eneo hili lina ekari 100. Ninaomba sana sisi tuwe walinzi wa vifaa hivi vilivyopo hapa ndani na kamwe tusishiriki mpango wowote wa kurudisha maendeleoa nyuma,” amesisitiza.

Naye, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali ya awamu ya sita ndani ya mwaka mmoja imetoa sh. bilioni 51.4 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za Taifa na Kanda. “Kwa ajiili ya Hospitali za Mikoa nchi nzima, Rais wetu ametoa shilingi bilioni 54.2 na kwenye eneo la vifaa, ndani ya mwaka huu mmoja ametoa shilingi bilioni 290.9,” alisema.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange amesema jengo hilo lililozinduliwa ni miongoni mwa majengo 80 yaliyojengwa nchini kwa kutumia fedha za UVIKO-19. Katika mkoa wa Lindi, majengo kama hayo yamejengwa pia katika wilaya za Liwale na Kilwa.

Amesema katika awamu ya kwanza, wilaya hiyo ilipokea sh. bilioni 2.9 ambazo majengo yake yamekamilika na sasa Rais Samia Suluhu Hassan ameleta sh. milioni 800 za kujenga wodi za kisasa ambazo zitakuwa na vifaa vya kisasa pia.

Mapema, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Salvio S. Wikesi alisema mradi huo  unatarajiwa kuwa na majengo 22 ambayo hadi kukamilika kwake yanatarajiwa kugharimu sh. bilioni 7.5.

“Hospitali  inaendelea na ujenzi wa majengo matano ya awamu ya tatu ambayo ni jengo la huduma za dharura, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la wodi ya upasuaji wanaume na wodi ya upasuaji wanawake.”

“Hadi sasa, mradi umegharimu kiasi cha shilingi milioni 390.72 ikiwa ni ongezeko la vifaa na kiasi cha shilingi milioni 90.72 ambazo zimetumika kuimarisha eneo la hospitali kwa kuwa lilikuwa na maji mengi chini ya ardhi na hivyo maandalizi ya ujenzi kuanzia hatua ya msingi hadi jamvi yalihitaji uimarishaji msingi wa jengo.”

Amesema pamoja na ukamilishaji wa jengo hilo, Serikali pia ilitoa vifaa tiba vya kisasa na Wizara ya Afya ikapeleka mashine ya x-ray, mashine ya kutakasia vifaa kabla ya kufanya upasuaji na mashine ya kumfanya uangalizi mgonjwa wakati wa upasuaji

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…