

BRYSON MSHANA
Ni washiriki wa mashindano ya michezo ya shule za msingi nchini Tanzania (UMITASHUMTA) ambayo yalihusisha mikoa yote ya Bara na Visiwani.
Mashindano haya yanafanyika kitaifa mkoani Tabora ambapo yalianza Julai 29,2022 na kumalizika Agusti 9,2022.
Mashindano haya yaliendana na burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi ambao walisheheni vipaji vya ushangiliaji na hamasa ya hali ya juu pale timu zao zilipokuwa viwanjani.
Wapo ya wahamasishaji waliotia fora ambao licha ya kuondolewa katika baadhi ya michezo katika hatua za mwazo, lakini bado uwepo wao unatambulika na kuwapa burudani washiriki waliosalia katika michuano pamoja na watazamaji wengine.
Si wengine hawa ni wanafunzi wenye amsha amsha ya aina yake ambayo waliyafanya mashindano ya UMITASHUMTA 2022 kuwa na ‘vibe’ lakini kwa mgeni anayefika uwanjani kwa mara ya kwanza ni ngumu kuamini kama wanafunzi hawa walishatolewa kwenye baadhi ya michezo.
Hawa ni wanafunzi wa kutoka mkoa wa Tanga unaosifika zaidi kwa kilimo cha matunda mbalimbali husan machungwa.
Wawapo uwanjani wanafunzi hawa wavulana kwa wasichana kazi yao ni moja tu kushangilia mwanzo mwisho bila kujali kama timu ya mkoa wao inacheza au haichezi ni kawaida kuwakuta kwenye uwanja mmojawapo wakionesha uwezo wao wa ushangiliaji.
Ushangiliaji wao haubagui mshindi wala mshindwa wao kazi yao ni kucheza ngoma asubuhi mpaka jioni kwa kuhakikisha wanatembea kila uwanja wenye mchezo wowote kwa wakati husika.
Utawakuta na mavazi yao nadhifu ya rangi ya bluu isiyokolea sambamba na waalimu wao wa ushangiliaji wakiwa wameunda umbo la duara wanazunguka na kuimba nyimbo za makabila ya mkoa wa Tanga.
Rajab Dimosso ni Mratibu UMITASHUMTA Mkoa wa Tanga, katika mahojiano maalumu na mwandishi wetu anasema kiasili Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa ambayo wakazi wake ni wachangamfu,hivyo pamoja na maandalizi ya michezo wanafunzi wakiwa kambini waliandaliwa katika eneo la hamasa.
“Mkoa wa Tanga uchangumfu ni asili yetu, hata wakati wa maandalizi hatukuishia tu kwenye kujiandaa kimchezo tu bali pia suala la hamasa kwetu lilikuwa kipaumbele kikuu ndio maana umeuona huo uchangamfu wa wanafunzi wetu na waalimu wao,”anasema Rajab Dimosso.
Dimosso anasema baadhi ya michezo michezo walifika robo fainali kama Netball,Goalball (Uliohusisha watu wenye uono hafifu, mpira wa wavu na mpira wa mikono (Handball) lakini na hivyo kupata vikombe vya ubingwa nidhamu na usafi na kuwa nafasi ya pili katika sanaa za michezo upande wa ngoma, nafasi ya tatu Goalball.
“Hakurudi Tanga watupu tulipata jumla ya medali mbili za dhahabu, moja ya fedha na tatu za shaba katika mchezo wa riadha kundi maalum kwa hiyo unaweza kuona hapo kuwa licha ya kuwa vizuri kwenye uhamasishaji lakini pia michezoni hatukuwa nyuma,” amesema Dimosso.
Dimoso ameongeza kuwa ushangiliaji wao wa mwaka huu ulijielekeza zaidi kwenye uhamasishaji wa zoezi la sensa ya watu na makaazi linalotarajiwa kufanyika Agusti 23, 2022 huku akisema walipata zawadi ya ushangiliaji ambayo iliambatanishwa katika kikombe cha nidhamu na usafi.
Walimu waliokuwa wanaongoza wanafunzi hao katika hamasa ni Amim Kibinda kutoka Shule ya Msingi Mkata Mkata Halmashauri ya Handeni Vijijini, Omar Kingwaba wa Shule ya Msingi Chanika Halmashauri ya Handeni Mji na Miraji Mwewale anafundisha shule ya Msingi Manundu mazoezi iliyopo Halmashauri ya Korogwe Mji Mkoani Tanga.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Walimu Amin Kibanda, anasema kuwa anapenda sanaa na UMITASHUMTA ilihusisha sanaa na michezo hivyo alishirikiana na wenzake kuhakikisha kuwa wanauwakilisha vizuri mkoa wa Tanga.
“Kama ulisikia siku mashindano haya yanafunguliwa na Naibu Katibu mkuu anayeshughulikia Elimu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, Dkt Charles Msonde alieleza kuwa lengo la michezo hii ni kukuza michezo na sanaa katika shule na Taifa kwa ujumla, ndicho tunachokifanya mkoa wa Tanga” anaeleza Mwalimu Amin Kibanda.
Mashindano ya UMITASHUMTA 2022 amabayo yanahusisha michezo mbalimbali yalifunguliwa julai 29, 2022 na Naibu Katibu mkuu anayeshughulikia Elimu OR – TAMISEMI, Dr. Charles Msonde.
Augusti 04, 2022 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alizindua rasmi mashindano hayo akisisitiza juu ya Serikali kuunga mkono michezo mashuleni.
Mashindano ya UMITASHUMTA & UMISETA mwaka 2022, yalindaliwa na kusimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaana Michezo.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…





