BRYSON MSHANA, MTWARA

Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameahidi kuwa serikali itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo bure kwa wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza kilimo na kuongeza kipato cha wakulim a vijijini.

Dkt. Nchimbi alitoa ahadi hiyo Tarehe 02 Octoba 2025, alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi katika mikutano minne ya kampeni iliyofanyika katika wilaya za Mtwara, Tandahimba, na Newala.

Alieleza kuwa serikali ya CCM imejipanga kuendeleza huduma kwa wakulima kwa kuhakikisha kuwa pembejeo muhimu kama vile mbolea, viuatilifu, na mbegu bora zinapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu – au bure kabisa kupitia ruzuku.

“Zao la korosho limekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa mikoa ya kusini, hasa Mtwara na Lindi. Hatuwezi kuwaacha wakulima peke yao. Tutaendelea kuwapatia pembejeo bure, na kuhakikisha wanawezeshwa kulima kwa njia za kisasa zitakazoongeza tija na mapato,” alisema Dkt. Nchimbi huku akishangiliwa na umati wa wananchi.

Mbali na suala la pembejeo, Dkt. Nchimbi pia alieleza kuwa serikali itawekeza katika ujenzi wa visima vipya vya maji kwa ajili ya skimu za umwagiliaji, hasa katika maeneo ya Nanguruwe, Tandahimba, na Newala, lengo ni kusaidia wakulima kulima mara mbili au zaidi kwa mwaka, na kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara hauathiriwi na mabadiliko ya tabianchi.

“Tutaimarisha miundombinu ya umwagiliaji, kuongeza ruzuku ya mbolea na pembejeo, na kuwafikia wakulima kwa karibu. Hii ndiyo njia ya kweli ya kuinua uchumi wa wananchi wetu walioko vijijini,” alisisitiza Dkt. Nchimbi.

Katika mikutano hiyo, wagombea ubunge wa CCM kutoka majimbo mbalimbali walipata nafasi ya kueleza mafanikio ya serikali ya awamu iliyopita na kuahidi kusimamia utekelezaji wa miradi iliyobaki.

Abdala Chikota (Nanyamba), Arif Premji (Mtwara Vijijini), Yahya Nawanda (Newala Vijijini), na Ahmed Katani (Tandahimba) waliwahakikishia wananchi kuwa wataendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha changamoto zote zilizobakia zinapatiwa suluhisho la haraka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Said Nyengedi, alimhakikishia Dkt. Nchimbi kuwa wananchi wa Mtwara wamejipanga kuhakikisha CCM inapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao.

“Tumeona kazi iliyofanywa. Wananchi wetu wanatambua hilo, na watakipa CCM ushindi wa kishindo Oktoba 29,” alisema Nyengedi.

Ziara hiyo ya kampeni ni sehemu ya mwendelezo wa Dkt. Nchimbi kukutana na wananchi wa mikoa ya kusini – Mtwara na Lindi – kwa lengo la kuzinadi sera za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…