BRYSON MSHANA, MTWARA

Bandari ya Mtwara imefanikiwa kuongeza kiwango cha ufanisi katika kuhudumia shehena ya korosho baada ya kufanikisha usafirishaji wa jumla ya tani 370,896 katika msimu wa 2024/2025, ikilinganishwa na tani 253,616.94 za msimu wa 2023/2024.

Taarifa hiyo imetolewa tarehe 29 septemba 2025, na Meneja wa Bandari ya Mtwara Ferdinand Nyathi, katika mkutano wa wadau wa Bandari uliofanyika kwenye Ukumbi wa Benki Kuu – Mtwara, ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi na Mwenyekiti wa mkutano huo.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliyowasilishwa na Meneja wa Bandari ya Mtwara Ndg. Ferdinand Nyati, ongezeko hilo ni sawa na 46.2%, na limevuka lengo la kuhudumia tani 200,000 pamoja na makadirio ya uzalishaji wa tani 300,000 yaliyotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania.

“Msimu wa 2024/2025: hadi Machi 31, 2025, jumla ya tani 370,896 za korosho zilihudumiwa na kusafirishwa nje ya nchi, Msimu wa 2023/2024, jumla ya tani 253,616.94 zilihudumiwa,hii ni sawa na ongezeko la 46.2%, na kiwango hicho kilipita lengo la TPA la tani 200,000 na hata kuzidi makisio ya uzalishaji wa tani 300,000” ameeleza nyathi.

Kuhusu Changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita ameeleza kuwa ni pamoja na upungufu wa mitambo, ufinyu wa maeneo ya kuhifadhia shehena, na msongamano wa meli. Hatua zilizochukuliwa na Bandari ni pamoja na kuongeza mitambo mipya, kutenga maeneo ya ziada ya kuhifadhia korosho, na kupanga kipaumbele kwa meli zilizokuwa tayari kupakiwa.

Taarifa hiyo imeelezea pia mikakati ya Msimu wa 2025/2026, ambapo Bandari ya Mtwara imejipanga kusafirisha zaidi ya tani 367,264 za korosho sambamba na makisio ya uzalishaji wa tani 700,000.

Aidha Bandari ya Mtwara itaendeleza mafunzo kwa wafanyakazi na wateja ili kuongeza uelewa wa mifumo mipya, kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika ufungashaji wa shehena nje ya eneo la bandari, utumia mtambo mpya wa SSG uliosimikwa Juni 2025 pamoja na mikataba ya kukodisha mitambo ya ziada na kuendeleza punguzo la tozo za kuhudumia mizigo na masharti nafuu ya kuhifadhi makasha.

Kwa upande wake Serikali ya Mkoa wa Mtwara imewataka wadau wote wanaohusika kwenye usafirishaji wa zao la korosho ghafi kufuata maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha korosho zinazozalishwa mikoa ya kusini Lindi, Mtwara na Ruvuma zinasafirishwa kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) mkoani Mtwara.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema maagizo ya serikali lazima yafuatwe kwani korosho kupitia bandari ya mtwara kwenda kwenye masoko ya nje kunaongeza ajira na kukuza uchumi wa mkoa huo pamoja na mikoa jirani.

‘’Nitoe wito kwa wadau na taasisi zinazosafirisha korosho kuendelea kuzingatia maelekezo ya serikali ya kutumia bandari ya mtwara kusafirisha korosho zote za mikoa ya kusini Ruvuma, Lindi na Mtwara katika hili niwapongeze kwa ushirikiano huo, maelekezo hayajabadilika kwahiyo tuendelee kujipanga kwamba korosho zetu tunapoingia kwenye msimu kutoka mikoa yetu hii mitatu zitasafirishwa kupitia bandari ya mtwara’’amesisitiza Kanali Sawala

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…