Wakili wa Serikali Mkoa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Nunu T. Mangu akisoma Hotuba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini kwenye viwanja vya mahakama kuu, Mtwara Tarehe 03 Februari 2025.

BRYSON MSHANA, MTWARA

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeahidi kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi zinazohusika na haki madai pamoja na wadau wengine kama Mahakama, asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa na jumuiya za kikanda na kimataifa ili kuboresha utawala wa sheria na haki katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Ahadi hiyo imetolewa na Wakili wa Serikali Mkoa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Nunu T. Mangu wakati akisoma hotuba ya Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini kwenye viwanja vya mahakama kuu, Mtwara tarehe 03 februari, 2025.

Sambamba na hilo Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Serikai imependekeza, mfumo wa uendeshaji wa Mabaraza ya Kodi, Ardhi, Tume ya Ushindani, Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA) na taasisi nyingine za udhibiti, ufanyiwe maboresho ili kukabiliana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

“Kwa kuwa teknolojia ina nafasi kubwa katika kuifikia Tanzania ya 2050, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma za kisheria kwa kuweka mifumo madhubuti ya TEHAMA na kuweka msisitizo kwa Mawakili wa Serikali nchini kuendelea kujisajili na kuweka taarifa zao katika Rejesta ya Mfumo wa Taarifa za Mawakili (Office of Attorney General – Management Information System – OAG-MIS)”

“Mfumo huu wa OAG-MIS ulizinduliwa na Mheshimiwa Rais Dr. Samia  Suluhu Hassan mnamo  tarehe 29 Septemba, 2022 katika Mkutano wa Chama cha Mawakili wa Serikali ulifanyika jijini Dodoma” ameeleza Wakili Nunu T. Mangu

Ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni mahakama ya Tanzania imepiga hatua katika kuboresha utoaji haki kwa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kujenga vituo jumuishi vya utoaji haki, kujikita katika matumizi ya TEHAMA katika kutoa haki na kupunguza hatua za kusikiliza mashauri ya madai kutoka hatua 38 mpaka kufikia 21.

Amesema huo ni mchango mkubwa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,  kwani linachangia kuvutia biashara na uwekezaji hapa nchini.

“Ni katika misingi hiyo hiyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kutafuta fedha za Kuendeleza ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Taasisi za Kisheria (Government Legal Institutions Integrated Centers-GLIICs) katika Mkoa wa Mwanza na Arusha”

“Ujenzi wa majengo haya ukikamilika utasogeza huduma karibu na wananchi na utasaidia utekelezaji wa majukumu ya taasisi zetu kwa mujibu wa Katiba na sheria, kurahisisha utendaji kazi, kupunguza gharama za uendeshaji wa ofisi, kutoa haki kwa wakati na kuondoa migongano ya maslahi na wadau mbalimbali”

Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Sheria Nchini yalifanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali Jijini, Dodoma tarehe 03 Februari, 2025 na kuhudhuriwa na Mgeni rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Dkt. Samia  aliitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha inaendelea kuzingatia masilahi ya nchi kwenye Mikataba mbalimbali ambayo nchi inakusudia kuingia kwakua Kikatiba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo yenye dhamana ya Upekuzi na Tathimini ya Mikataba inayongiwa na Serikali na Taasisi zake.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…