MUSSA MTEPA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas, amewataka Wanahabari kuzingatia weledi kwenye kuchapisha habari ikiwa ni pamoja na kutoandika habari za upande mmoja wa chanzo.

Kanali Abbas ametoa rai hiyo Novemba 20, 2023 wakati wa hotuba ya uzinduzi wa Jukwaa la Habari na Mawasiliano Mkoa wa Mtwara, lililoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC).

“Tujitahidi sana kuepuka migongano ya kimasilahi kati yetu na wadau wa habari tunaofanya nao kazi, lakini jambo la pili ni kuepuka kuandika habari zenye nia ya uchochezi na uchonganishi.”

Aidha, amewapongeza Wanahabari wa Mkoa wa Mtwara kwa kazi wanayoifanya kuuhabarisha umma juu ya matukio ya Mkoa huo.

Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda, akaeleza umuhimu wa jukwaa hilo katika kuimarisha uhusiano baina ya wanahabari na taasisi zilizopo ndani ya Mkoa wa Mtwara.

Kwa upande wake Katibu wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mtwara ameelezea umuhimu wa jukwaa hilo kuwa litazidi kuwaunganisha waandishi wa habari na wadau katika mkoa huo, hali ambayo itazidi kuondoa changamoto za utoaji wa taarifa hususan katika Taasisi za Serikali.

“Jukwaa hili ni endelevu, tumezindua leo lakini tutaendelea kuliboresha na litakuwa linafanyika kila mwaka kwa kuzingatia mzunguko wa kuzifikia wilaya zote, tunaishukuru sana ofisi ya mkuu wa Mkoa kwa kukubali wazo hili na kulifanyia kazi” ameeleza Mshana

Jukwaa hilo limehusisha Wanahabari wote wa Mkoa wa Mtwara, Maofisa Habari wa serikali ngazi za halmashauri na taasisi mbalimbali pamoja na wakuu wa taasisi.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…