HAIKA KIMARO, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Wakati Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) ikitarajia kutoa matokeo ya awamu ya pili ya chanjo ya majaribio ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ifikapo Juni 2024, matumizi ya dawa ya kufubaza virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa baadhi ya wanawake wanaofanya biashara ya ukahaba imeendelea kuwa changamoto.

Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa ambayo baadhi ya wanawake wanafanya biashara ya ukahaba hivyo kuhatarisha usalama wa afya zao na wateja wao na kusababisha kuenea kwa maambukizi mapya ya VVU.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara wanawake 16 kati ya 209 wanaofanya biashara ya ukahaba wamebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Akizungumza na MTPC Blog katika zoezi la kupima VVU katika kijiji cha Msijute Halmashauri ya Mtwara, Mratibu wa kudhibiti magonjwa ya Ukimwi na kupambana na maambukizi ya VVU kwa jamii kutoka halmashauri hiyo Dkt. George Mutangwaba anasema iliwachukua muda mrefu kuwashawishi wanawake wanaofanya biarasha ya ngono kujitokeza kupima afya zao kutokana na usiri uliogubikwa katika bishara hiyo.

“Jitihada kubwa imefanyika kwanza kuwatambua, pili kuwahamasisha wapime afya zao kwa hiyari…kwa wale ambao wana maambukizi tunawaanzishia dozi ya ARVs, hata hiyo changamoto kubwa hawahudhurii kliniki kikamilifu” alibainisha Dkt. Mutangwaba na kuongeza kuwa

“Wengi hawapendi kufika vituoni na hupenda usiri hivyo inatupa wakati mgumu kuwasimamia katika matumizi ya dawa, pia kwa kawaida wanawake hawa huwa wanahama hama kutoka wilaya moja hadi nyingine kutegemea na upepo wa kibiashara hasa wakati wa msimu wa mavuno ya mazao kama korosho, ufuta na mbaazi”

Mratibu huyo alifafanua kuwa “Unakuwa ushamuibua lakini kumsimamia kwenye dawa inakuwa shida kwa sababu leo atakuwa Masasi, kesho Mtwara vijiji biashara ikiwa ngumu atahamia Mtwara Manispaa ila kumbuka ulikuwa ushamsajili kwa hiyo inakuwa ngumu katika kuwabaini na kuwafuatilia.”

Ametaja umri wa wanawake wengi wanaojihusisha na biashaa ya ngono na ukahaba kuwa ni kati ya miaka 18-30, umri ambao unatajwa kuwa na wateja wengi.

“Wengi ni wenyeji wa huku lakini baadhi wanakuja huku msimu wa korosho, ufuta na mbaazi, ikishaisha hiyo wengi wao wanarudi nyumbani, walio wengi wanafanya biashara hii ili kujipatia fedha ya kukidhi mahitaji yao, mtu anaona bora auze mwili kuliko kuuza nyanya,”anasema Dkt. Mutangwaba

Mmoja wa wasichana waliokutwa na maambukizi baada ya kupimwa kipitia mradi wa ‘Afya yangu’ wa EPIC KOKODA unaolenga kufikia makundi maalumu ikiwemo, wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili na wasichana wa rika balehe amelazimika kupima afya kutokana kujihusisha kimapenzi na wanaume tofauti bila kutumia kinga.

“Roho ilikuwa inadunda sana kwa sababu ya hofu kwani tunakopita wengi hawaaminiki na wengine huwa hawataki kutumia kinga hivyo nakubaliana nao wanavyotaka,”anasema

Maneno Jumbe (sio jina lake halisi) ni kijana anayejihusisha na mapenzi ya jinsia moja anasema kwa sasa ataondokana na biashara hiyo baada ya kupewa elimu.

Mtaalamu wa maabara kutoka Halmashauri ya Mtwara Sofia Nasibu anasema wakati wa upimaji wa VVU katika kijiji cha Msijute, wananchi watatu kati ya 98 waliojitokeza kupima wamekutwa na maambukizi ya VVU.

“Wengi wamejitokeza walikuwa wanataka kujua hali ya afya zao, wengine walikuwa na wasiwasi na mashaka lakini baada ya kupima wamejua nini cha kufanya ili wasipate maambukizi na kwa wale wenye maambukizi watapewa utaratibu wa kuanza dawa za kufubaza maambukizi,” anasema Sofia

Mkurugenzi wa Shirika la Faidika Wote Pamoja (FAWOPA) Baltazari Komba, anasema ili kuwa na muendelezo mzuri kwa wanaotumia dawa za kufubaza VVU ni vyema zikianzishwa ‘mobile clinic’ ambazo zitamuwezesha mtumiaji yeyote kupata huduma sahihi popote tofauti na sasa mtumiaji anatakiwa kuchukilia katika eneo alilojisajilia kutokana na watu kuhama hama kwa sasa kwa sababu mbalimbali.

Anasema Serikali na wadau wanaweza kuangalia namna wanavyoweza kusimamia kesi za mtu kupata huduma popote ili mradi awe na kadi yenye namba maalumu ambayo akienda sehemu ya kutolea huduma namba hiyo itatumika na taarifa zake zote zitapatikana.

“Utaratibu wa kugawa dawa (ARV’s) umekaa kiimla sana kwamba kama unachukua dawa labda zahanati fulani au kituo fulani lazima uchukulie hapo hapo.. kwa sasa hivi jinsi watu wanavyohangaika duniani inakuwa ngumu sana, mobile clinic inaweza kuwa suluhisho,”anasema Komba

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…