BRYSON MSHANA, LINDI
0787 569 833
Agusti 04, 2023 Wizara ya Mali Asili na Utalii ya Tanzania iliandaa siku ya utalii, uhifadhi na utunzaji wa mazingira ikiwa ni sehemu ya maonesho ya wakulima Nanenane Kanda ya Kusini katika viwanja vya Ngondo Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi.
Siku hii ilikuwa na dhumuni la kuikumbusha na kuihamasisha jamii juu ya usimamizi, utunzaji na uhifadhi wa mali asili za nchi, ili kuendelea kuwa na mazingira rafiki kwa utalii na kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi.
Mkuu wa Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara Alhaji Mwangi Rajab Kudya, alishiriki katika siku hiyo iliyoandaliwa kwenye eneo la Banda la Mali asili na Utalii, akiwa ndiye mgeni rasmi akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara, Kanali Patrick Sawala.
Akizungumza baada ya kupata maelezo juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Mali Asili kupitia Taasisi zake kama Wakala Wa Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Alhaji Kudya alisisitiza juu ya jamii kuendelea kuelimishwa juu ya faida zinazopatikana kupitia uhifadhi.
“Taifa linapata faida kubwa kutokana na uhifadhi ikiwepo upatikanaji wa hewa safi,Mvua za kutosha, Mazingira mazuri, misitu, kuongezeka kwa wanyamapori pamoja na kuingiza fedha za ndani na za kigeni kupitia utalii”
“Niwapongeze sana Wizara ya Mali asili kwa kuandaa siku hii hapa kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya kusini, hii inasaidia kukumbushana juu ya umuhimu wa kutunza rasilimali zetu ili kuepukana na majanga yanayoweza kusababisha mabadiliko ya Tabia nchi” alisema Alhaji Kudya.
Pamoja na hayo, pia aliitaka Jamii na mamlala zilizopewa dhamana ya kulinda mali asili nchini kutekeleza wajibu wao, ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na maeneo mengi yanayofaa na kuvutia kwa ajili ya utalii na pia kuhamasisha wananchi kufanya utalii wa ndani.

Awali akitoa maelezo kwa mgeni rasmi juu ya shughuli za uhifadhi wa wanyamapori, Afisa Msaidizi Daraja la Pili kutoka Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Kusini Mashariki Bi. Ruth Palangyo alieleza kuwa wanaendelea kuhifadhi maeneo mbalimbali kwa ajili ya utalii na uwekezaji.
Bi Ruth alieleza kuwa maeneo ya kuwekeza kwenye sekta ya utalii kwa Kanda ya kusini bado yanapatikana na taratibu zimewekwa juu ya wale wanataka kupata vibali kwa ajili ya shughuli mbalimbali zinazoruhusiwa kufanyika kisheria katika hifadhi hizo.
“Mikoa hii ya kusini ina utajiri mkubwa wa mali asili mbalimbali, sisi kama Mamlaka ya uhifadhi wa Wanamapori tunavyo vivutio vingi katika maeneo tunayoyasimamia na tunaendelea kuwasisitiza wadau mbalimbali kutembelea lakini pia kuwekeza kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa” ameongeza Bi. Ruth
Kwa upande wake Mhifadhi kiotengo cha Ugani na Uhamasishaji kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya kusini Bw. Hashim Kitivo, aliwataka wananchi kutochoma misitu ili kutunza mazingira kwa ajili ya ufugaji wa nyuki na wanyama wengine.
“Bado tuna changamoto ya wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi kufanya uharibifu hasa wa kuchoma miti jambo ambalo linachangia uharibu wa mazingira na kufukuza viumbe hai wanaotumia misitu kama makaazi yao ya kudumu”
Nao Wananchi mbalimbali waliofika kushuhudia siku hiyo ya ya usimamizi, utunzaji na uhifadhi wa mali asili walieleza kufurahishwa na utaratibu huo wa Wizara ya Mali Asili na Utalii kwani imewasaidia kuapata elimu sambamba na kugawiwa miti bure kwa ajili ya kwenda kupanda kwenye maeneo yao.
“Ukifika hapa unapata elimu ya mambo mbalimbali ya utalii na mali asili, unapewa mpaka Asali bure ili uone umuhimu wa kutunza misitu, lakini kama hiyo haitoshi tumepewa na miti bure twende kupanda katika mazingira yetu tunayoishi” alieza Halima Ally Mkaazi wa Kijiji cha Madangwa Mkoani Lindi.
Siku ya utalii, uhifadhi na utunzaji wa mazingira iliyoadhimishwa Agusti 4, 2023 ikiandaliwa Wizara ya Mali Asili na Utalii ya Tanzania, wakati maonesho ya wakulima Nanenane Kanda ya Kusini katika viwanja vya Ngondo Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi, inaonesha kwa vitendo juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzani kupitia Wizara husika katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na mazingira bora ya Utalii nchini.
Hali hii itaendelea kuvutia watalii katika vivutio mbalimbali nchini, na kuzidi kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii nchini ambayo yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 714.59 kwa mwaka 2020 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 1,310.34 (zaidi ya Sh trilioni 3.05 mwaka 2021).
SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI USHIRIKI WA WADAU KATIKA MAENDELEO YA MAKAZI NCHINI
Na Munir Shemweta Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ushiriki wa wadau katika…






