BRYSON MSHANA, LINDI
mtwarapressclub@gmail.com
Wananchi katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma wamekuwa wakihamasika kulima zao la ufuta kwenye maeneo mbalimbali, hali inayoelezwa kuwa inatokana na kuimarika kwa bei ya soko ya zao hilo katika masoko ya vyakula Duniani.
Muamko huu wa Wakulima kuanza kutumia utaalamu katika kilimo cha ufuta tija katika mazao yao sambamba na ongezeko la uzalishaji jambo ambalo litaenda sambamba na kuongezeka mauzo na kipato kwa wakulima na Serikali.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi Zainab Telak Agusti 01, 2023 wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo Lindi, ilionesha kuwa zao la ufuta limeendelea kuingiza fedha kwa wananchi na Serikali.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa msimu uliomalizika wa 2023/2024 zao la Ufuta lilifanya vizuri katika mikoa ya Mtwara na Lindi, kwa kuuza Jumla ya Tani 67,705 (Mtwara 15,691 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 58.5 na Mkoa wa Lindi, Tani 52,014 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 193.5).
Kwa upande wa mkoa wa Ruvuma, Takwimu za Chama kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) Mkoa ulivuka lengo la ukusanyaji wa Ufuta kwa zaidi ya asilimia 20.37% msimu 2023/2024 kutoka lengo la kilo 3,822,561 hadi kufikia kilo 4,800,997.20 huku mauzo yakifikia Shilingi Bilioni 17.6.
Mafanikio haya katika soko, yamepelekea kuendelea kuongezeka kwa jitihada za kuwekeza kwenye utafiti na uzalishaji wa mbegu bora za ufuta, ili wananchi wanaoshiriki kilimo hicho wawezeshwe kulima kisasa na kwa tija itakayopelekea kuongeza uzalishaji.
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini TARI Kituo cha Naliendele Mtwara, imewekeza katika kutafiti pamoja na kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali kama Korosho, Ufuta, Karanga, Mihogo, Matunda pamoja na Mbogamboga, hivyo kuwa msaada kwa wakulima wanaolima mazao hayo nchini.
Zabron Ngamba ni Mtafiti wa Zao la Ufuta kutoka TARI – NALIENDELE, ambaye ameeleza kuwa pamoja na wananchi wengi kujitokeza kulima ufuta, lakini bado wanatakiwa kusisitizwa juu ya utumiaji wa mbegu bora ambazo zitawasaidia kuongeza uzalishaji na kwa wakati sahihi.
“Ufuta unalimwa kwa ajili ya chakula lakini pia kuuza kwa jili ya kupata kipato, na katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wananchi wanaoingia katika kilimo hicho, hivyo sisi kama wataalamu tunalo jukumu la kuwasaidi na kuwaongoza katika kuendelesha kilimo bora”
“Muamko ni mkubwa, oda za mbegu za kisasa tunazozalisha TARI nazo zimeongezeka kwa wakulima mmojammoja na Taasisi kutoka mikoa ya Kusini, Kati na Nyanda za juu Kusini” ameeleza Ngamba.
Ngamba amesema kuwa kuongezeka kwa mahitaji ya Mbegu za Ufuta ni fursa kwa wazalishaji wa Mbegu, hivyo kuwataka Wananchi na Taasisi mbalimbali kujifunza kuzalisha mbegu bora za ufuta ili waweze kuziuza na kujiongezea kipato.
“Hii ni fursa nyingine, kilo moja ya Mbegu bora ya Ufuta inauzwa hadi Shilingi 6,500/= na ianaweza kupandwa kwatika shamba la zaidi ya eka moja kwa kufuata kanuni za kilimo bora, kwa hiyo niwaombe wale wanaotaka kujifunza uzalishaji wa mbegu za ufuta wafike TARI wapate muongozo”
Kwa upande wa Wakulima wa Ufuta wanaeleza umuhimu wa kuzingatia kilimo bora na ushauri kutoka kwa wataalam ili kuzidisha uzalishaji.
Bi Zaituni Malonda Mkulima kutoka kijiji cha Tunduru ya Leo, Selelmani Mkilumwile wa Kijiji cha Mkotokwiano wote kutoka wilayani Nachingewa Mkoani Lindi, na Abdallah Yusuf kutoka Mnazi Mmoja Lindi, ni baadhi ya wakulima ambao walitembelea maonesho ya Wakulima na wafugaji Nanenane kwa ajili ya kushiriki shmba Darasa la ufuta linalosimamiwa na TARI kwenye viwanja vya Ngongo Lindi.
“Tupo hapa kupata elimu ili tukalime ufuta kisasa na kuongeza uzalishaji ili tupate kipato kikubwa, mimi nimesafiri kutoka Wilayani Nachingwea nimefika hapa kujifunza kilimo Bora cha ufuta, hii ni bahati kubwa kwetu, nawasisitiza wakulima wenzangu washiriki mashamba darasa ili wajifunze na kuona faida yake” amongeza Bi Zaituni Malonda
Wakati Kanda mbalimbali nchini zikiendelea na maonesho ya wakulima na wafugaji nanenane ambayo kitaifa yanafanyikia Jijini Mbeya, ni wakati wa wakulima kuendelea kutumia muda huu katika kujifunza mbinu bora za kilimo kupitia wataalam mbalimba ili waweze kufanya kilimo cha manufaa kitakachowapa chakula pamoja na fedha.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






