BRYSON MSHANA, LINDI

www.mtwarapressblog.co.tz

Mikoa ya Mtwara na Lindi imepongezwa kwa maandalizi mazuri ya Maonesho ya Wakulima na wafugaji, Nane nane Kanda ya Kusini, yaliyofunguliwa rasmi tare 1 Agusti 2023 kwenye viwanja vya Ngongo Manispaa ya Lindi.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sigini, akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, akisisitiza kuwa ameshuhudia maboresho makubwa kwenye maeneo yote aliyotembelea na mazingira ya uwanjani kwa ujumla.

Akizungumzia Maadhimisho ya Sikukuu ya Nanenane ya mwaka 2023 yaliyobeba Kaulimbiu inayosema, Vijana na Wanawake, ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula amaesema yamejielekeza katika kuendeleza nia nzuri ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda,

“Bajeti ya Serikali mwaka 2023/2024, imejikita zaidi katika kuboresha huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo za uhakika, kuvutia uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi zinazotoka na kilimo, mifugo, uvuvi, nyuki na misitu”

“Hali hii itasaidia kuongezeka kwa masoko ya bidhaa ndani na nje ya nchi na hivyo kuwahahakikishia wakulima bei nzuri na za uhakika kwa mazao yao” Ameeleza Naibu Waziri Jumanne Sigini.

Awali akitoa salama za mikoa ya Lindi na Mtwara kwa mgeni rasmi,  Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi Zainab Telak, alizungumzia namna ambavyo serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka juhudi katika kukuza kilimo na ufugaji kwa mikoa ya kusini.

Amesema kuwa Serikali imewezesha ujenzi wa kituo cha kuzalisha vifaranga za mazao ya bahari chenye thamani ya Shilingi Milioni 800 Halmashauri ya Mtwara.

“Ujenzi mwingine ni wa bandari ya Uvuvi yenye thamani ya Bilioni 266, Halmashauri ya Kilwa, na pia tunatarajia kukopeshwa boti 49 za uvuvi wa kina kirefu (Mtwara 18 na Mkoa wa Lindi 31) ameeleza RC Zainab.

Maonesho ya Kanda ya Kusini yanajumuisha Wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali, Mashirika ya Serikali na Binafsi, Mashirika na Jumuia zisizokuwa za Serikali (NGOs), Jumuia na Asasi mbalimbali za kijamii (CBOs), Makampuni na watu binafsi pamoja na wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…