MWANDISHI WETU

mtwarapressclub@gmail.com

Shirika la Madini la Taifa(STAMICO)limeandaa mkutano wa siku mbili unaolenga kujadili changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini nchini, unaotarajiwa kufanyika  Aprili 5 na Aprili 6, 2023, Jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa  Waziri wa Madini  Dkt. Dotto  Biteko.

Hayo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt  Evance  Mwese wakati akizuungumza na na waandishi wa habari Aprili 04, 2023 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo.

Ameeleza kwamba mkutano huo utafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere( JNICC) Dar es salaam na utawakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo wachimbaji wa madini ya malighafi za viwandani,wamiliki wa viwanda ,pamoja na taasisi za kifedha(Bank).

Dkt  Mwese amesema mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha wachimbaji wadogo wa madini kutoka mikoa mbalimbali ukiwa na shabaha ya kuvifanya viwanda  vya madini vifanye kazi kwa ufanisi ili kuzalisha bidhaa za bei nafuu na kuweza pia kushindana na soko la dunia.

” Wenye viwanda njooni ili mtoe changamoto zenu tufahamu  nini hasahasa kinawakwamisha kutumia malighafi za hapa nchini,hii itatusaidia sisi kama shirika la Madini la Taifa kuchukua hatua za kuondoa changamoto hizo na kukuza sekta ya viwanda kama serikali ilivyoweka agenda ya kuhakikisha kuwepo kwa uchumi utokanao na  viwanda” amesema Dkt Mwasse.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini( CTI) Leodigar Tenga amesisitiza watu wenye viwanda kujitokeza kwa wingi ili kujadili kwa pamoja changamoto zinazowakabili ili waweze kutumia malighafi za viwandani zilizopo hapa nchini.

“Napenda nisisitize kwamba nchi yetu inataka ijenge uchumi wake kutokana  na viwanda,tuna Madini yetu  nchini ,tuna wajibu sisi kama Cti kuhamasisha watu wenye viwanda kutumia malighafi tulizonazo hapa nchini kwani wenye viwanda wanataka kuwepo na upatikanaji wa malighafi kwa wingi pamoja na ubora” amesema Tenga

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Wadogo Mkoa wa Dar es salaam na Pwani ( DACOREMA) Josephat Mkombachepa pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Wanawake Wachimba Madini Tanzania( TAWOMA) Salma Ernest wameishukuru serikali kupitia STAMICO kwa kuandaa mkutano huo kwani utawasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili.

Mkutano huo pia utazishirikisha taasisi za udhibiti ikiwemo Mamlaka ya Mapato (TRA), Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira( NEMC), Tume ya  Madini inayosimamia masuala ya leseni kwa wachimbaji wa madini pamoja na Maabara za Kupima Ubora wa Madini.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…